Welcome to Souq commerce Store !
Mada ya 4: Maandalizi ya Ufugaji Kuku wa Asili

Mada ya 4: Maandalizi ya Ufugaji Kuku wa Asili

Size :
(0 customer review)
Ili uweze kufuga kuku wa Asili kwa faida, ni vyema kufanya maandalizi ya awali yatakayokuwezesha kuzalisha kuku walio bora. Maandalizi hayo yanajumuisha utayarishaji wa banda kulingana na idadi ya kuku utakaofuga, uchaguzi wa kuku bora na uandaaji wa vifaa vya kulishia au kutagia na uwiano wa kuku ndani ya banda.


Banda bora:
Ni muhimu kuwajengea kuku banda bora ili wapate kujikinga na mvua, baridi, wezi na wanyama. Banda la kuku linaweza likajengwa kando kando au nyuma ya nyumba ya kuishi. Eneo linapojengwa banda la kuku pawe:
i. Panafikika kwa urahisi.
ii. Pasituamishe maji.
iii. Pasiwe pa mwelekeo wa upepo mkali.

Banda la kuku linaweza kujengwa kwa kutumia raslimali za misitu zinazopatikana kwa urahisi kwenye eneo husika. Vifaa muhimu katika ujenzi wa banda ni pamoja na miti, nyasi, mabati, makuti,
fito, udongo, mabanzi, saruji na vifaa vingine mbalimbali vya ujenzi.


Sifa za banda bora la kuku:
i. Liwe na paa imara lisilovuja.
ii. Kuta zisiwe na nyufa kama umetumia tofali (zisilibwe au zipigwe lipu) kwani nyufa ni maficho ya      wadudu kama viroboto, utitiri, chawa nk.
iii. Sakafu isiwe na nyufa au mipasuko.
iv. Liwe na madirisha ya kutosha kupitisha hewa.
v. Liwe na uwezo wa kuingia mtu wa kufanya usafi na huduma nyingine muhimu.
vi. Liwe na ukubwa (nafasi) unaolingana na idadi ya wastani wa kuku 10-15 kwa mita moja mraba           kwa kuku wanaofugwa huria, ili wawe na nafasi ya kulala tu wakati wa usiku. Ila kwa kuku                 wanaofugwa kwa mfumo wa nusu ndani nusu nje wanastahili eneo la mita moja mraba kwa
viii. kuku 4 - 5 ili kuruhusu nafasi ya vyombo vya chakula na maji.


Kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi:
Mafanikio zaidi katika kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi yatapatikana iwapo uchaguzi na uchambuzi wa kuku wanaozaliwa utafanywa mara kwa mara. Sababu kubwa ya kufanya uchaguzi ni kupata kundi la kuku litakalofaa kwa sifa zote katika uzalishaji. Sifa hizo ni pamoja na kupevuka haraka, kutaga mayai mengi, kuwa na uzito mkubwa na nyama nyingi kwa umri mdogo. Ufugaji bora utazingatia kuchagua kuku wenye sifa nzuri na kuwaacha waendelee na uzalishaji na wanaosalia wauzwe au waliwe.

Vilevile kuku wa Asili wanaweza kuboreshwa zaidi kwa kutumia majogoo ya kisasa kama vile
Rhode Island Red-RIR ili kupata kuku wanaokua haraka wenye uzito mkubwa na kutaga mayai
mengi zaidi.


Sifa za kuzingatia wakati wa kuchagua mitetea:
Wawe na:
i. Umbile kubwa.
ii. Uwezo wa kutaga wakiwa na umri mdogo (miezi 6).
iii. Uwezo wa kustahimili magonjwa.
iv. Uwezo wa kukua haraka.
v. Uwezo wa kutaga mayai mengi {zaidi ya 15 kwa mtago mmoja (clutch)}.
vi. Uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi na kuwalea.


Sifa za kuzingatia wakati wa kuchagua majogoo:
Jogoo bora, awe na:
i. Umbo kubwa.
ii. Miguu imara na yenye nguvu.
iii. Kucha fupi.
iv. Mwenye nguvu.
v. Machachari.
vi. Upanga/kilemba kikubwa.
vii. Uwezo wa kuitia chakula mitetea.
viii. Tabia ya kupenda vifaranga.


Njia zitumikazo katika kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi:
i. Kwa kuangalia kuku wenyewe kulingana na sifa zilizotajwa hapo juu.
ii. Kwa kufuatilia kumbukumbu za wazazi wa kuku unaotaka kuwachagua.
iii. Kwa kuangalia kumbukumbu za familia (wazazi, kaka na dada).
iv. Wakati muafaka wa kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi:
v. Mara tu wakitotolewa.
vi Wakati wa ukuaji.
vii. Zoezi endelevu.
viii. Uzalishaji ukishuka chini ya asilimia 50.
ix. Wakati kuku wanapoangusha manyoya.


Faida ya kuondoa kuku wasiofaa kwenye kundi:
i. Inasaidia kuongeza uzalishaji wa mayai.
ii. Inapunguza kulisha kuku ambao uzalishaji wake ni hafifu.
iii. Inapunguza uenezaji wa magonjwa ya kuku.
iv. Huongeza nafasi zaidi kwa kuku wazuri kwenye banda.
v. Uwezekano wa kuuza kuku kama hao ni mkubwa kabla hawajafa.


Umri wa kupevuka:
i. Mitetea huanza kutaga wakiwa na umri wa miezi 6 - 8.
ii. Jogoo huanza kupanda akiwa na umri wa miezi 7 lakini mbegu zake huwa bado kukomaa.
iii. Hutoa mbegu zilizokomaa anapofikia umri wa miezi 10.


Muhimu: Ni vizuri jogoo atumike kwa miaka mitatu tu ili kuepuka mchanganyiko wa damu kwa wenye nasaba moja kwani kufanya hivyo husababisha uzalishaji duni. Kama umeamua kufuga kuku wa mzao wa kwanza (F1) ni vyema kuwapandisha mitetea hao (F1) kwa majogoo ya asili ili kuendeleza damu ya asili. 


Uwiano wa mitetea na majogoo:
Ili kudumisha amani katika kundi la kuku, na ili kupata mayai yenye mbegu ya jogoo ambayo yana uwezo wa kutoa vifaranga ni muhimu kuangalia uwiano kati ya mitetea na majogoo. Sio sahihi kuweka mitetea wengi kwa majogoo wachache na majogoo wengi kwa mitetea wachache. Uwiano unaokubalika ni wastani wa jogoo mmoja kwa mitetea kumi hadi kumi na mbili {1: 10-12}.


Fuga kuku upate faida kwa kuzingatia:
i. Elimu na Ushauri kutoka kwa mtaalamu wa mifugo na kutimiza yafutayo:
ii. Chanjo ya mdondo kila baada ya miezi 3.
iii. Chanjo ya ndui mara 2 kwa mwaka.
iv. Zuia viroboto, utitiri na minyoo.
v. Chagua mayai bora kwa ajili ya kuatamiza.
vi. Panga kuuza kuku kwa makundi uongeze kipato.
vii. Boresha lishe ya familia kwa kula mayai na kuku.
viii. Gawa mapato yatokanayo na ufugaji wa kuku kwa matumizi yako (33%), maendeleo ya mradi
       (33%), na akiba (33%).



USIKOSE........................ Mada ya 5: Vifaa Muhimu Ndani ya Banda la Kuku

Kusoma mada iliyopita bofya HAPA

Kutota@Heifer International Tanzania

Clothing & Apparel:

Jewelry & Watches:

Health & Beauty: